Mwanafunzi wa darasa la tatu alifariki Jumatatu huku wengine weninge wakiendelea kupokea matibabu katika hospitali ya wilaya ya Molo baada ya kugongwa na gari mjini Molo.
Walioshuhudia ajali hiyo wamesema dereva wa gari aina ya Nissan linalomilikiwa na shule ya Jubilee Elite Academy alipoteza mwelekeo na kugonga wanafunzi waliokuwa wakitembea kando ya barabara kwenda shuleni.
John Towett, ambaye ni mmoja wa walioshuhudia ajali hiyo amesema visa vya watu kugongwa na magari vimeongezeka mjini Molo, huku akiitaka mamlaka inayosimamia barabara kutenga nafasi maalum ya watu kupitia ili kuepukana na ajali za mara mara.
Akidhibitisha ajali hiyo, Kamanda wa trafiki wilayani Molo Nderitu Maina amesema uchunguzi wa ajali hiyo umeanzishwa huku akiwataka madereva kuwa wangalifu ili kupunguza visa vya ajali.
Mkuu huyo wa trafiki amesema wanamzuilia dereva wa gari hilo huku akisubiri kufikishwa mahakamani.
Huzuni ilitanda katika shule ya msingi ya Kambala baada ya wanafunzi na waalimu kupata habari kuhusiana na ajali hiyo na kifo cha msichana huyo wa darasa la tatu.
Mwili wa mtoto huyo umehifadhiwa katika ufuo wa hospitali ya wilaya hiyo.