Wanafunzi wa shule ya upili ya Rigogo Chonjo ambayo ni ya kutwa, waliandamana Jumatatu usiku wakielekea katika hospitali ya Maili Kumi kumpeleka mmoja wao ambaye wanasema aliumizwa na waalimu wawili mwendo wa saa kumi, kwa kupigwa.
Aidha kulingana na wanafunzi hao walisema waliandikisha taarifa katika kituo cha polisi cha Maili Kumi Bahati, wakisema sio mara ya kwanza kwa waalimu hao wawili kuwapiga kitutu kwa madai ya kukosa nidhamu, na sasa wanataka idara ya elimu iweze kuingilia kati.
Huku wakiimba nyimbo za kukejeli dhuluma dhidi ya wanafunzi, walisema wataandamana hadi wapate haki.
Mmoja wao Samwel Mbugua, alisema tatizo lilianza mwendo wa saa kumi jioni Jumatatu, wakati ambapo mwalimu mmoja aliyemtambua kama bwana Theuri, aliingia darasani kidato cha nne akapata halijafagiliwa, na alipotaka kujua ni kwa nini halijafagiliwa, mwanafunzi huyo akasema yeye hakujua kama alifaa kufagia siku hiyo.
Hapo ndipo alipigwa na waalimu hao wawili, na sasa wanasema kwamba mwanafunzi huyo amefura mbavu na kichwa kutokana na kichapo alichokipata.
Walisema kwamba Mwalimu mkuu pamoja na naibu wake walikuwa hawako kitendo hicho kikitokea.
Akidhibitisha hayo chifu kata ya Kirima Charles Macharia, amesema alijaribu kuzungumza na wanafunzi hao warudi nyumbani lakini hakufaulu. Alikemea kitendo hicho.