Watu wawili wamepoteza maisha yao katika visa viwili tofauti kwa njia tatanishi mjini Naivasha, na Mai Mahiu.
Katika kisa cha kwanza, wakazi wa eneo la Sanctuary lililoko kando ya ziwa la Naivasha wameachwa na wasi wasi baada ya mwanamke mmoja kugongwa na nyaya za umeme alipokuwa akifua nguo.
Mfanyikazi huyo wa kampuni moja ya maua alikuwa akianika nguo zake wakati mkasa huo ulimpata.
Kwingineko mjini Mai Mahiu, mfanyibiashara mmoja mashuhuri amejitoa uhai katika kisa kisichoeleweka.
Mfanyibiashara huyo mwenye umri wa miaka 50 na ambaye anamiliki shule moja ya kibinafsi anaaminika kuchukua hatua hiyo baada ya kukosana na mkewe.
“Tulipata mwili wake kama unaning’inia kwenye paa la nyumba yake,” mkazi mmoja kwa jina Joseph Njoroge amesema.
OCPD wa Naivasha Titus Munyoki amedhibitisha matukio hayo, huku akisema kuwa miili hiyo imechukuliwa na kupelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali kuu ya wilaya ya Naivasha.