Mwanamke anayekabiliwa na shtaka la kumuuwa mumewe eneo la Kisauni mwaka wa 2013 amekanusha kuhusika na mauaji hayo katika mahakama kuu ya Mombasa.
Mshukiwa, Agnes Mutheu, anadaiwa kumdunga mumewe, Antony Mutheu, kisu cha paja, mnamo Machi 16, 2013 katika eneo la Kisauni.
Akitoa ushahidi huo wakati wa kujitetea kwake siku ya Jumanne, Mutheu aliambia mahakama kuwa alimpenda mumewe na alishtuka alipomuona amedungwa kisu pajani ndani ya chumba chao cha kulala.
Mutheu alisema kuwa mumewe alikuwa mlevi kabla ya kifo chake na kusisitiza kuwa mwendazake alikuwa na desturi ya kumpiga akiwa mlevi.
Aidha, ripoti ya uchunguzi inaonyesha kuwa marehemu aliuwawa kwa kuvuja damu kwa wingi, hali iliyosababishwa na jereha la kisu.
Mahakama kuu inatarajiwa kutoa hukumu yake Disemba 10, 2015.