Wakazi wa mtaa wa Kihoto viungani mwa mji wa Naivasha walipigwa na butwaa Jumamosi baada ya mwanamke mwenye umri wa makamo kumdunga mumewe kwa kisu na kumuua kufuatia malumbano kuhusiana na uhusiano wa kimapenzi nje ya ndoa almaarufu, ‘mpango wa kando.’
Hali ya huzuni ilitanda zaidi katika kisa hicho cha Jumamosi polisi walipofika na kuuchukua mwili wa mwanamme huyo ambaye ni mfanyikazi wa shamba moja la maua lililoko mjini humo huku wakimkamata mkewe na kumpeleka katika kituo cha polisi cha Naivasha.
Inaarifiwa mwanamke huyo alimshuku mumewe kuwa na uhusiano na mwanamke mmoja anayefanya kazi naye katika shamba hilo la maua na kutelekeza familia yake changa.
Mkaazi mmoja aliyeshuhudia tukio hilo Jane Wangari alisema kuwa kwa miezi kadhaa iliyopita, wapenzi hao walikuwa wamezozana kuhusiana na mume kuwa na uhusiano nje ya ndoa na mwanamke uyo huyo huku mkewe akitishia kuondoka katika ndoa hiyo.
“Wakati wa tukio hilo, huyu mwanamme alianza kumchapa mkewe ambaye anadaiwa kumdunga kwa kisu kikali kwenye kifua huku wanao wawili wakitazama,” Wangari alisema.