Mwanamme mmoja katika kaunti ya Nakuru alihukumiwa kifungo cha maisha na mahakama ya mji huo, kwa kumdhulumu kimapenzi bintiye mwenye umri wa miaka sita unusu.
Katika uamuzi wake Jumanne, hakimu mkaazi wa Nakuru Judicaster Nthuku alisema kwamba mwanamme anayembaka mtoto wake mwenyewe, anamwondolea ubikra wake na kumwachia shida ya kukumbuka alichopitia.
“Mshtuko wa mwili unaweza kuondoka, lakini wa kimawazo unasalia maishani mwa mtoto huyo daima, mbakaji kama huyo hastahili kuonewa huruma, anastahili kifungo cha maisha,” Nthuku alisema.
Mhukumiwa Anthony Kyalo Mutemila alikuwa ameshtakiwa kumbaka bintiye wa miaka sita unusu mnamo mwezi Julai 16, 2014 mwendo wa saa nne unusu usiku katika mtaa wa kwa Rhonda kaunti ya Nakuru.
Katika ushahidi wake, mtoto huyo alieleza mahakama kwamba alikuwa akilala kwenye kiti wakati babake aliingia nyumbani akiwa amebeba tochi na soda, na mara moja akaanza kumtendea alichokiita ‘tabia mbaya’.
Aidha mahakama iliambiwa na mtoto huyo kwamba haikuwa mara ya kwanza kwa babake kumtendea unyama huo.
Mamake msichana huyo alisema kwamba ilikuwa mwendo wa saa nne unusu usiku alipogundua bwanake hajaingia kitandani, na alipotaka kujua mbona bintiye anasumbuka kwenye kiti, bintiye akamwambia kwamba babake anamtendea tabia mbaya.
Aliwasha stima na kumwona bwanake akivalia longi, ambapo alipiga kamsa iliyolazimisha bwanake kutorokea usalama wake, japo alisakwa na majirani hadi akakamatwa.
Katika kujitetea kwake, mshukiwa aliomba huruma akisema ana watoto wengine wanne na mwanamke tofauti.