Mwanamme mmoja ameshtakiwa katika mahakama moja ya mjini Kwale kwa madai ya kupatikana na ngozi ya nyoka aina ya chatu kinyume cha sheria.
Inasemekana kuwa mwanamme huyo aliyetambulika kama Bakari Mwanduri alikamatwa siku chache zilizopita na maafisa wa kulinda wanyamapori KWS katika eneo la Matuga akiwa na ngozi hiyo.
Inadaiwa kuwa mwanamme huyo amekuwa akifanya biashara ya uwindaji haramu na kwamba amekuwa akiuza bidhaa hizo haramu ambazo zinaaminika kuwa ghali mno.
Kukamatwa na kushtakiwa kwa mwanamme huyo kumekuja wakati huu ambapo mashirika mbalimbali yanajitokeza katika vita dhidi ya uwindaji haramu nchini ili kunusuru baadhi ya watu wanaaminika.
Kama ilivyo kwa bidhaa zingine zinazotokana na wanyamapori, ngozi ya nyoka pia inaaminika kuwa na thamani kubwa katika masoko ya ng’ambo hivyo kufanya watu wengi kuingilia biashara hiyo haramu.
Wadau mbalimbali katika sekta ya utalii duniani wamekuwa wakipinga vikali uwindaji haramu huku wakisema kwamba hatua hiyo huchangia pakubwa kudidimia kwa biashara hiyo ya utalii.
Sheria za humu nchini zinasema kuwa mtu anayepatikana na makosa ya uwindaji haramu anaweza kutozwa faini ya hadi shilingi milioni 100 au kifungo cha miaka 15 gerezani.
Hata hivyo Bakari alikana madai hayo mbele ya hakimu mkuu wa mahakama hiyo Cosmas Maundu, na kesi hiyo itatajwa tarehe 17 mwezi Februari na kuskizwa tena tarehe 2 April.