Share news tips with us here at Hivisasa

Maafisa wa polisi mjini Nyamira wameanzisha uchunguzi wa kubaini chanzo cha mwanamume wa umri wa miaka 68 kujinyonga katika kijiji cha Nyagwere, eneo bunge la Borabu.

Akithibitisha kisa hicho, naibu chifu wa eneo hilo Agnes Ondieki alisema mwendazake alijifungia chumbani mwake na kujinyonga bila ya jamaa zake kujua siku ya Jumamosi jioni.

Alisema kuwa tayari maafisa wa polisi wameupeleka mwili wa mwanamume huyo kwenye hifadhi ya Hospitali kuu ya Nyamira.

"Marehemu alipatikana akiwa amejinyonga chumbani mwake na tayari maafisa wa polisi wameuondoa mwili wake katika eneo hilo na kuupeleka kwenye hifadhi ya Hospitali kuu ya Nyamira," alisema Ondieki.

Afisa huyo wa utawala aidha amewahimiza wakazi wa eneo hilo kutafuta ushauri wanapokumbwa na matatizo ya maisha badala yao kuamua kujitoa uhai.

"Kuna mashirika mengi ambayo yanaweza kutoa ushauri mtu anapohisi amezidiwa na mawazo. Ni himizo langu kwenu kutafuta ushauri mwafaka badala yakuamua kujinyonga,” alihimiza Ondieki.

Visa vya watu kujinyonga katika Kaunti ya Nyamira vimekuwa vikiripotiwa kwa siku za hivi karibuni, hali inayoibua maswali kuhusu kiini cha visa hivyo.