Share news tips with us here at Hivisasa

Mwanamume wa miaka 41 kutoka kaunti ndogo ya Yatta amepoteza maisha yake baada ya kuangukiwa na jiwe alipokuwa akichimba mawe.

Akidhibitisha kisa hicho siku ya Jumatano, naibu wa chifu wa Elumanthi Philip Maingi alisema kuwa mwanamume huyo alikuwa kati ya wanaume watano waliokuwa wakichimba mawe katika machimbo hayo kabla ya janga hilo kutokea.

Chifu huyo alielezea kuwa huenda kisa hicho kilisababishwa na mvua kubwa inayoshuhudiwa katika eneo hilo.

"Wanaume hao walikuwa katika shughuli za kuchimba mawe ambayo baadaye huuzwa kwa wateja, pale jiwe kubwa kutoka ukutani mwa chimbo hilo lilimwangukia mwanamume huyo aliyeaga dunia papo hapo,” alisema Maingi.

Vilevile, Maingi aliwaomba wafanyakazi katika machimbo ya mawe kusubiri hadi msimu was mvua kupita ili kurejelea kazi yao kutokana na hatari iliyomo msimu huu wa mvua.

Maingi alielezea kuwa kisa cha aina hiyo kilishuhudiwa hivi majuzi katika eneo la Kisiiki, mwamume mmoja alipoangukiwa na jiwe na kujeruhiwa.