Mwanamume mmoja anakabiliwa na shtaka katika mahakama moja mjini Garissa kwa madai ya kumvunja mkewe mkono kufuatia ugomvi wa kinyumbani.
Mwanaume huyo, Yussuf Mohamed Ali, 45, kutoka eneo la Shabah, kaunti ya Garissa amemvunja mkono mkewe baada ya kuliasi amri yake ya kuwapeleka ng'ombe malishoni asubuhi wa siku ya Alhamisi na kupelekea maafa hayo.
Mke wake, Halima sheikh Hassan,38, anapokea matibabu katika hospitali kuu ya Garissa huku akiwa katika hali isiyoridhisha.
Akiongea na wanahabari akiwa kwenye hospitali hiyo, Bi Halima alisema kuwa, alivunjwa mkono na mume wake kufuatia ugomvi wa kinyumbani kuhusiana na malisho ya ng'ombe.
"Alinimbia nipeleke ng'ombe malishoni na nikakataa amri yake kwa kuwa nilikuwa mgonjwa. Hakutaka kusikia shida zangu na nikiwa naosha vyombo ndipo aliponigonga na rungu iliyokuwa karibu yake na kunivunja mkono wangu wa kulia," alisema Halima.
Bi Halima anaeleza kuwa, hio sio mara ya kwanza tukio kama hilo kutokea baina yake na mumeo, akitaja matukio mengine mawili yaliyotokea awali, lakini hakupata jeraha lolote wala maumivu, ingawa alimzaba makofi hafifu shavuni.
"Kunazo mara mbili nyingine alinizaba makofi hafifu hafifu shavuni lakini hayakuniathiri vyovyote," alisema Halima.
Wazee wa kijiji hicho walijaribu kulitatua shida hiyo kijamii lakini mkewe akadinda na kumpeleka mumewe mahakamani ili aweze kupata haki yake na mumewe kufunguliwa mashtaka.
Kwa sasa, mwamaume huyo yupo korokoroni akisubiri kufikishwa mahakamani hivi karibuni kujibu shtaka linalomkabili.