Mwasiasa mmoja kutoka eneo la Pwani ambaye anapania kuwania kiti cha ubunge cha Mvita Fadhiha Awadh analitaka shirika la feri kuyakagua magari kabla ya kuingia kwenye feri ili kuepuka visa vya malori ya mizigo ambayo yamekuwa yakisababisha ajali kwenye kivuko hicho.
Akiongea siku ya Jumanne katika afisi yake iliyoko katikati ya jiji la Mombasa, Fadhiha alisema kuwa itakuwa vyema zaidi iwapo shirika la feri litachukua hatua hiyo, na itawapunguzia misongamano ikizingatiwa kuwa malori hayo mara nyingi hukwama na kuzuia magari mengine kuingia na kuwaharibia biashara pamoja na kuwacheleshea wateja wao kufika mahali pao pa miadi.
Mwanasiasa huyo alisema kuwa wakati umefika shirika hilo kuwa katika mstari wa mbele kuboresha huduma zao badala ya kila mara kuwa katika zogo la wateja na watumiaji wa feri na kujaribu kutafuta ushauri kutoka kwa wataalamu wengine ili kupata maarifa zaidi ya kuliendeleza shirika hilo vyema zaidi kuliko ilivyo sasa hivi.
“Mimi mwenye nimeponea mwishoni mwa mwezi wa Oktoba baada ya lori kutoka barabarani na kupoteza breki na kuingia upande mwingine wa bahari,” alisema kiongozi huyo.
Alisema haya baada ya lori kupoteza udhibiti wake na kugonga gari moja kwa upande na dereva na kulielekeza baharini, hali ambayo hata wakazi wamekuwa wakilalamikia kuwa huenda lori jingine likajipata katika hali hiyo na kuwagonga watu wakati wanakimbilia kuingia au kutoka kwenye feri.