Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mwanaume mmoja alikesha katika kituo cha polisi cha Solai usiku wa kuamkia Jumanne baada ya kumuuwa mkewe katika kijiji cha Banita kata ya Ndungiri Jumatatu jioni mwendo wa saa kumi na mbili.

Akidhibitisha kisa hicho chifu mkuu wa Kata hiyo Tony Kurui, amesema akiwa na maafisa wa polisi kutoka ktuo cha polisi cha Solai Waliupata mwili wa mwanamke huyo ukiwa na majeraha mabaya kichwani ambapo wanashuku huenda mwanaume huyo alitumia kifaa butu kumgonga kichwani.

“Tuliupata mwili wa mama huyo ukiwa na majeraha mabaya sehemu ya kushoto wa kichwa chake, kumaanisha mumewe alimgonga kwa kifaa butu,” Kurui alisema.

Aidha amesema mwanaume huyo alikimbilia usalama wake katika kituo hicho cha Solai baada ya wakaazi wenye gadhabu kumtimua mbio wakitaka kumuadhibu.

“Nusra mwanaume huyu auawe na umma kutokana na hasira waliokuwa nayo, ni bahati nzuri kwa kuwa alijipeleka katika kituo cha polisi.” Aliongeza chifu huyo.

Hata hivyo wakaazi wa eneo hilo wamedokeza kwamba mwanaume huyo amekuwa na mzozo na mkewe kwa muda, ambapo wanadai huenda ndio umepelekea mauaji hayo.

“Mwanaume huyu amekuwa akizozana na mkewe kwa muda mrefu na kabla kumuua mkewe waligombana kwa muda mrefu,” alisema jirani wao mmoja ambaye alitaka jina lake kubanwa.

Kwa sasa mwili wa mwanamke huyo umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti mjini Nakuru.