Share news tips with us here at Hivisasa

Mwendeshaji pikipiki mmoja anaendelea kuuguza majeraha katika hospitali moja mjini Mombasa baada ya kudungwa kisu na wahalifu wanaodaiwa kumvamia siku ya Alhamisi.

Watu wanaoaminika kuwa wezi wa pikipiki wanadaiwa kumkabili mwendeshaji huyo kwa nia ya kumpora lakini akakataa kusalimu amri na kupelekea yeye kupata majeraha hayo.

Polisi ambao walikuwa wanashika doria katika eneo hilo la Approved katika kaunti ya Likoni walifika upesi baada ya kupigiwa simu na kumkimbiza hospitalini kwa huduma ya kwanza.

Hata hivyo, waendeshaji pikipiki wenzake waliungana na kuanzisha msako wa dharura mara moja na kufanikiwa kuwakamata washukiwa 2 ambao wanadaiwa kuwa kwenye genge hilo la uhalifu.

Waendeshaji hao wakati huo huo wamevitaka vikosi vyote vya usalama kuwahakikishia usalama wao kwani biashara hiyo huwa ina changamoto si haba kando na kuhatarisha maisha yao katika pilka pilka za kutafuta riziki.

Wawili hao wamepelekwa katika kituo cha polisi cha Likoni wakisubiri kufikishwa mahakamani mnamo siku ya Jumatatu. Wananchi wote wameombwa kutahadhari hasa wakati huu wa sherehe nyingi hususan nyakati za usiku.