Mwanamme mmoja mwenye umri wa makamo aliuawa kwa kugongwa na gari kwenye barabara kuu ya Nairobi kuelekea Nakuru Jumapili usiku.
Mwili huo ulipatikana mapema Jumatatu ukiwa kando ya barabara katika kijiji cha Laini yapata kilomita kumi kutoka mjini Naivasha.
Mkaazi mmoja Jackson Mwaniki alisema mwanamme huyo alikuwa ameonekana Jumapili mchana akiwa mlevi, kabla ya kupatikana amefariki kwa kugongwa na gari.
Polisi wa kituo cha Naivasha walichukua mwili huo na kuupeleka katika hifadhi ya maiti ya hospitali ya wilaya mjini humo.
Barabara kuu ya Nairobi-Naivasha-Nakuru hadi Eldoret, imekuwa kero kubwa kwa wanaoitumia, huku maafa yakiripotiwa kila wiki.
Maeneo ambayo yametambuliwa kama hatari kwenye barabara hiyo, ni ikiwemo Kinungi, Flyover pamoja na eneo la Salgaa.