Mwenyekiti wa mamlaka ya kupambana na dawa za kulevya na pombe nchini Nacada, ameitaka mamlaka ya usalama na usafiri wa barabarani NTSA, kuweka bango kubwa la kutahadharisha madereva kutokiuka sheria za trafiki katika eneo la Salgaa.
Kwenye kikao na wanahabari siku ya Jumatatu mjini Naivasha, John Mututho alisema kuwa hatua hiyo itasaidia kupunguza ajali zinazotokea eneo hilo mara kwa mara.
Haya yanajiri siku chache tu baada ya ajali mbili kutokea tangu mkesha wa mwaka mpya na kusababisha maafa ya watu saba.
Mututho alipendekeza ujenzi wa barabara hiyo kuangaliwa upya kwa kusema hali ya barabara hiyo kwa sasa imechangia ongezeko la ajali.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa shirika hiyo ya Nacada imeiandikia barua mamlaka ya NTSA kuhusiana na swala hilo jambo ambalo hadi wa sasa halijafanyika.
Hata hivyo, Mututho ametaka uchunguzi dhabiti kufanyika ili kubaini ikiwa aliyekuwa akiendesha gari lililosababisha ajali eneo la Teachers na kuua wanafunzi watano mkesha wa mwaka mpya, alikuwa na leseni.