Share news tips with us here at Hivisasa

Kwa mara nyingine tena wanasiasa wa Mombasa wameonywa dhidi ya kutumia maneno ya uchochezi kwenye majukwaa.

Akizungumza na wanahabari siku ya Ijumaa, Naibu kamshina wa Kaunti ya Mombasa Salim Mahmoud, aliwahimiza viongozi kutotumia maneno ambayo yanaweza kuleta uhasama miongoni mwa wananchi, ikizingatiwa uchaguzi mkuu wa 2017 unawadia.

Mahmoud alisisitiza kuwa kiongozi atakayepatikana akitoa matamshi hayo atakabiliwa kisheria pasi kujali cheo.

Hatua hii inajiri kutokana na joto la kisiasa linaloshudiwa katika Kaunti ya Mombasa, huku viongozi wa mirengo ya Jubilee na Cord wakionekana kuzozana kuhusu jinsi ya kuendeleza taifa.

Wakati huo huo, Mahmoud amewatahadharisha wazazi ambao watoto wao wanajihusisha na visa vya uhalifu na kuwataka kushirikiana na watoto wao ili kuwajenga kimaadili.