Huku seneta wa Kaunti ya Mombasa akitangaza rasmi kuwa atawania wadhifa wa ugavana katika Kaunti hiyo, Mbunge wa Mvita Abdulswamad Sharrif Nassir amesema kuwa hana nia yoyote ya kuwania kiti cha useneta wala cha ugavana.
Nassir amesema kuwa kwa sasa atabakia kwenye kiti cha ubunge na kuendelea kuwawakilisha wananchi katika eneo bunge la Mvita na kuhakikisha kuwa anakamilisha miradi yote pamoja na kutimiza ahadi zote alizotoa kwa wenye wakati alipokuwa akifanya kampeni za nafasi ya ubunge.
Akiongea siku ya Jumatano na waandishi wa habari katika Kaunti ya Mombasa kwenye eneo bunge lake, mbunge huyo alisema kuwa kila mtu ana haki ya kuwania kiti chochote cha siasa ambacho anaona kinamfaa na kuwafaa wale anao wawakilisha.
Kuhusiana na seneta wa kaunti hiyo kutangaza kumpinga gavana wa sasa Ali Hassan Joho kwenye uchaguzi mkuu ujao, Nassir aliweka wazi kuwa kila mmoja ana nafasi ya kikatiba kufanya uamuzi ambao anaona ni mwafaka kwake, hivyo haoni kosa lolote kwa Omar kuchukua hatua hiyo kwa vile uamuzi ni wake binafsi.
Hata hivyo, kiongozi huyo aliweka bayana azima yake ya kupigania kiti cha ugavana katika Kaunti ya Mombasa ifikapo mwaka wa 2022, ana akawataka wananchi kuwa tayari kumpigia kura wakati ukitumia wa kupiga siasa za kaunti hiyo za ugavana.