Share news tips with us here at Hivisasa

Wakaazi katika eneo la Likoni wameishtumu wizara ya kushughulikia majanga, dharura na mipangilio maalum katika Kaunti ya Mombasa wakidai imewatenga kwa kukosa kukarabati miundo msingi ili kukabiliana na  mvua ya El Nino.

Wakaazi wanasema mvua hiyo itaendelea kusababisha hasara kubwa kwenye maeneo mengi  kaunti hiyo kwani hakuna mikakati iliyowekwa kukabiliana na athari zake.

Wakiongozwa na mzee wa mtaa  Kibuyuni Salim Mwanyoa, walisema kuwa serikali ya Kaunti ya Mombasa imekosa kuwashughulikia kupunguza athari za El nino licha ya  serikali ya kitaifa na ya kaunti kutenga fedha za dharura ya El nino.

Mwanyoa alisema kuwa hawajaona lolote likifanywa na tume teule ya Kaunti ya Mombasa ambayo iliwajibishwa kukabili makali ya mvua hiyo ambayo wakazi wengi wanasema imewasababishia mabadiliko makubwa kwenye taratibu zao za kutafuta riziki.

“Hii mvua ukiangalia jana pekee yake iliweza kung’oa vibanda vya wafanyabiashara wa rejareja na kusababisha wengi hata kupoteza mali  kadhaa , hata sasa hivi unaona biashara nyingi hazijafunguliwa,”  Mwanyoa alisema.

Aidha mzee huyo aliongeza kuwa mahali kwingi hasa barabara za kuingia mitaani hazipitiki kwa sababu ya mafuriko.

Mzee huyo ambaye alikuwa akiongea na mwandishi  huyu  Jumatano huko Likoni, alitoa wito kwa serikali kuu kufanya uchunguzi wa kina na kubaini jinsi hela hizo zilizotengewa majanga ya mvua ya El Nino zimeweza kutumiwa na Kaunti zote nchini.