Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Baraza la makanisa nchini tawi la North linataka shughuli ya kuchukua silaha ambazo zimo mikononi mwa wananchi bila kibali katika eneo hilo kufanya kwa makini.

Baraza hilo limesema ili kuhakikisha kuwa shughuli hiyo inafanywa kwa njia nzuri kwa kuzingatia haki za kibinadamu baraza hilo linataka lihusisishwe.

Mshirikishi wa baraza hilo Dan Kimutai alisema iwapo viongozi wa makanisa watapuuzwa katika shughuli hiyo ni bayana kwamba haitafaulu.

Akihutubu katika warsha ya amani ya NCCK mjini Eldoret ambayo iliwaleta pamoja viongozi wa kidini kutoka katika kaunti za North-Rift ikiwemo Turkana na Pokot Magharibi Kimutai alisema viongozi wa kidini kutoka maeneo hayo wana usemi mkubwa kwa wenyeji hivyo basi wanapaswa kuhusishwa katika shughuli hiyo.

Kwa mujibu wa Kimtai ni kwamba iwapo shughuli hiyo itaendelea kufanywa kiholela kama ilivyo kwa sasa haitaafikia matarajio yake.

“Kutwaa silaha kutoka kwa wananchi katika kaunti za Pokot na Turkana bila kuhusisha kanisa ni kazi bure, kuna haja ya viongozi wa kidini kuhusishwa katika shughuli hiyo ili kupata nia njema kutoka kwa wenyeji” alisema Kimutai

Bw Kimutai alitaka serikali kushirikiana na wadau wengine wote kukabiliana na uhasama kati ya jamii za Waturakana na Wapokot.

Kiongozi huyo alitaka swala la mipaka kati ya jamii hizo kushughulikiwa bila kuingiza siasa katika swala hilo.

Hata hivyo Kimutai alitaka mipaka ya tangu jadi kuheshimiwa ili kuepuka uhasama zaidi kati ya jamii za North-Rift.