Share news tips with us here at Hivisasa

Tume ya uiano na utangamano wa kitaifa imeelezea wasiwasi wake kuhusu kuendelea kuongezeka kwa uchochezi wa mitandaoni baina ya makabila tofauti nchini.

Afisa mkuu mtendaji wa tume hiyo Hassan Mohammed amesema kuwa kuendelea kukithiri kwa uchochezi wa mitandaoni ni hatari kwa taifa, haswa wakati huu taifa linapoelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2017.

Akizungumza Jumanee jioni katika hafla moja mjini Nakuru, Hassan alisema kuwa wakenya waliosoma na wanasiasa wamegeuza mitandao ya kijamii kuwa kumbi za malumbano ya kisiasa na kikabila .

Hassan aliongeza kuwa uchochezi unaoendelezwa mitandaoni ni hatari sana na unaweza kuliangamiza taifa.

“Kuna watu ambao wamegeuza mitandao ya kijamii kuwa kumbi za makabiliano ya kikabila na wanachochea makabila yao dhidi ya mengine, na hii ni hatari kubwa sana kwa umoja na usalama wa taifa la Kenya,” alisema Hassan.

“Iwapo watu hawa, wakiwemo wanasiasa, hawatakomeshwa basi huenda kukawa na mgawanyiko mkubwa katika taifa hili mwaka 2017 kwa sababu makabila yatainukiana na kuchukiana sababu ya siasa za uchochezi,” aliongeza.

Alisema NCIC itazidisha juhudi za kukabiliana na uchochezi ili kuhakikisha kuwa taifa linabaki kuwa moja hata baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2017.

“Sisi tutafanya kazi yetu lakini pia wanasiasa wana jukumu la kutekeleza kwa kukoma kuwachochea raia kwa misingi ya kikabila na kisiasa,” alisisitiza.