Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mbunge wa Bahati Kimani Ngunjiri kwa mara nyingine amemkemea kiongozi wa upinzani nchini Raila Odinga kwa kususia mwaliko wa tume ya kukabiliana na ufisadi, EACC, kuelezea anachokifahamu kuhusu sakata ya Eurobond.

Kimani, aliyekuwa akiongea Ijumaa katika kituo cha kibiashara cha Dundori kaunti ya Nakuru, alidai Raila anacheza siasa na mkopo wa Eurobond, akisema kwamba anayoyasema kinara huyo wa Cord hayafai kuchukuliwa kwa kuwa na uzito.

Mbunge huyo wa mara ya kwanza katika bunge la kitaifa aliongeza kwamba japo serikali ya kitaifa imejikakamua kupigana na ufisadi, wanaoikosoa ni lazima wawe tayari kuweka mezani ushahidi wa madai yao kuhusu kashfa za kifisadi.

Aidha, amesema kwamba mdhibiti wa bajeti pamoja na waziri wa hazina kuu wameorodhesha vyema matumizi ya pesa hizo kwenye wizara kadhaa kwa maendeleo ya Kenya.

“Raila kukataa mwaliko wa waziri Rotich na pia EACC ni dhihirisho tosha kwamba hana ushahidi wowote wa kudhibitisha madai yake,” alisema Ngunjiri.

Kimani alikuwa katika wadi hiyo ya Dundori kwenye mkutano na wanachama wa muungano wa watumizi wa msitu wa Dundori – DECOFA.