Share news tips with us here at Hivisasa

Gavana wa kaunti ya Kisii James Ongwae ameahidi kuekeza zaidi katika sekta ya afya katika eneo lake.

Ongwae alisema atahakikisha sekta hiyo imeimarishwa kwa kununua dawa za kutosha na mashine mbalimbali za matibabu katika hosptali za kaunti hiyo.

Gavana Ongwae aliyasema hayo ijumaa katika hospitali ya rufaa na mafunzo mjini Kisii wakati kamati ya afya katika bunge la kitaifa likiongozwa na James Nyikal lilizuru kaunti ya Kisii kwa shughuli za ukaguzi.

"Yale ambayo nimefanya kwa sekta ya afya hayajatosha, nitafanya mengine ili kuona kuwa wananchi wanafaidika kimatibabu wanapougua," gavana alisema.

Nyikal aliipongeza serikali ya Ongwae kwa juhudi zake za kuwekeza katika sekta ya afya.

Hata hivyo, mbunge huyo alisema ikiwa serikali zote za kaunti zingeekeza zaidi katika sekta hiyo, basi serikali ya kitaifa ingeongeza mgawo wa pesa za afya kwa kaunti.

Mbunge wa Mugirango Magharibi James Gesami ambaye ni mwanachama wa kamati hiyo alisema jambo la kusikitisha ni wakati habari zinaibuka kuwa mwananchi amepoteza maisha yake kwa ukosefu wa matibabu katika hospitali za umma.