Share news tips with us here at Hivisasa

Mbunge wa Nyali Hezron Awiti Bollo ametangaza kung’ang’ania kinyang’anyiro cha kiti cha ugavana wa kaunti ya Mombasa katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka wa 2017.

Akiwahutubia wakaazi wa eneo bunge lake huko Nyali mjini Mombasa siku ya Jumapili, Awiti alisema kuwa kujitosa katika kinyang’aniro hicho ni kutokana na msukumo kutoka kwa wakaazi wanaotaka kufanyiwa maendeleo zaidi.

Awiti aliwashtumu viongozi wa kisiasa kwa kueneza uvumi kuwa hajakomaa kisiasa na hivyo basi atakuwa mgombea mwenza wa atakayekubaliana naye kumuunga mkono katika uchaguzi mkuu ujao huku akisisitiza kuwa lazima mabadiliko ya kimaendeleo katika kaunti ya Mombasa kufanywa.

"Wale ambao wanasema mimi sijakomaa kisiasa tutapambana wakati wa debe siku ya uchaguzi kwa sababu lazima wakaazi wetu wapate maendeleo jinsi wanavyotaka maana hao ndio wanatuchagua sisi tuwawakilishe na kuwafanyia kazi," alisema Awiti.

Mbunge huyo wa Nyali alimuonya Gavana wa kaunti ya Mombasa Ali Hassan Joho kuwa muangalifu dhidi ya kuwaachilia askari wake wa kaunti na mamlaka makubwa inayochangia kuwadhuluma na kuwanyanyasa wakazi bila hatia.

Hata hivyo ameunga mkono juhudi za maafisa wa usalama chini ya Kamishna wa kaunti hiyo Nelson Marwa kuimarisha usalama zaidi wakati wa sherehe za sikukuu ya Krismasi na mwaka mpya.