Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Gavana wa kaunti ya Mombasa Ali Hassan Joho ameapa kusalia katika chama cha ODM licha ya kudai kupokea vitisho vya mara kwa mara kutoka kwa wapinzani wake.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari siku ya Ahlhamisi muda mchache tu baada ya kupokonywa walinzi wake, Joho alidai kuwa serikali inampiga vita kutokana na msimamo wake thabiti wa kuunga mrengo wa upinzani hususan baada ya kukiongoza chama cha ODM kupata ushindi katika uchaguzi mdogo wa eneo bunge la Malindi.

‘’Wacha waendelee, mimi nitasalia katika upande wa upinzani kuwatetea wachache wasio na usemi. Walinzi wangu wamenipokonya lakini nitasalia kuwa Joho,’’ alisema Gavana huyo.

Siku ya Alhamisi idara ya usalama iliwaondoa maafisa wa polisi takribani saba ambao wamekuwa wakimlinda Joho, siku moja tu baada ya mshirikishi wa usalama katika ukanda wa Pwani Nelson Marwa kuamuru walinzi wa magavana Joho na Jeffah Kingi wachukuliwe hatua.

Marwa alidai kuwa walinzi hao walihusika katika uvurugaji wa amani katika uchaguzi mdogo wa Malindi, ambapo mama mmoja alidaiwa kuvuliwa nguo na vijana mbele ya walinzi hao bila kuchukuliwa hatua zozote.

Kwa upande wake idara ya usalama ilisema kuwa maafisa hao wameondolewa ili wapelekwe kwa masomo Zaidi.