Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Tume ya kitaifa ya ardhi (National Land Commission) imewataka watu wote ambao wanamiliki vyeti bandia vya umiliki ardhi ya uma mjini Eldoret kurejesha vyeti hivyo ili wasamehewe.

Tume hiyo ilisema aslimia kubwa ya ardhi ya uma mjini Eldoret imenyakuliwa na watu binafsi.

Naibu mwenyekiti wa tume hiyo bi Abigael Mbagaya alisema ardhi nyingi ya uma ikiwa ni pamoja na ikulu ndogo ya Eldoret imenyakuliwa na watu binafsi.

Mbali na Ikulu ndogo, bi Mbagaya alisema cheti cha umiliki ardhi katika makao makuu ya kaunti ya Uasin-Gishu kimo mikononi mwa mtu binafsi miongoni mwa ardhi nyingine ya uma ikiwa ni pamoja na maeneo yaliotengewa watoto kuchezea.

“Walio na vyeti hivi bandia wavirejeshe kabla ya kufikiwa na mkono wa sheria. Kama uko juu ya ikulu hama, shule hama, juu ya barabara hama, stesheni ya polisi hama, hata tunasikia hii makao makuu ya kaunti mtu ana cheti cha umiliki ardhi. Hiyo haiwezi ikakusaidia. Rejesha cheti hicho mapema,” alisema.

Akihutubu mjini Eldoret wakati wa warsha kwa uma kuhusu unyakuzi wa ardhi, bi Mbagaya aliwataka walionyakua ardhi ya ikulu ndogo mjini Eldoret pamoja na ardhi nyingine ya uma kurejesha ardhi hiyo kabla ya kufikiwa na shoka la sheria.

Bi Mbagaya alisema tume yake itaweka wazi majina ya watu ambao wamenyakua ardhi hiyo.

Bi Mbagaya alisema wanyakuzi wa ardhi ya uma watachukuliwa hatua za kisheria bila mapendeleo.

Afisa huyo amefichua kuwa vyeti vya umiliki ardhi vya afisi nyingi za uma mjini Eldoret vimo mikononi mwa watu binafsi.