Share news tips with us here at Hivisasa

Zaidi ya maskwota 1,000 kutoka kaunti ya Nakuru wameichangamoto tume ya ardhi nchini NLC, kuharakisha mpango wa kuwapa makao.

Walilalama kwamba ‘wawekezaji binafsi’ wameanza kunyemelea kipande cha ardhi ya makaazi cha Chepkisa/Tachasis chenye ekari 600 katika eneo la kaunti ndogo ya Njoro, kwa nia ya kuwaondoa kwenye ardhi hiyo yenye utata.

Ardhi hiyo ilitolewa kwenye msitu wa Likia na awali ilikuwa imenuiwa kufaidi maskwota hao, lakini baadhi yao wakahamishiwa shamba la makaazi la Teret, huku wengine wakirejea kudai haki yao ya umiliki kwenye shamba la awali.

Hata hivyo serikali ilitupilia mbali ulowezi wao kufuatia mpango wa kuweka mipaka kwenye msitu wa Mau na kuutenganisha na mashamba ya ulowezi yaliyotengwa mwaka wa 1997.

Kulingana na mwenyekiti wa kikundi cha Koyumi Chepkisa Julius Sambu, watawala wa mikoa katika eneo hilo wamekosa kutoa suluhu.

“Tuna matumaini kwamba NLC itaweka kwenye gazeti la serikali kipande hiki cha ardhi kwa sababu hakimo chini ya ile ya msitu," Sambu alisema.

Kupitia kwa wakili wao Kiplenge & Kurgat, maskwota hao walitishia kumshtaki yeyote anayehitilafiana na mpango unaoendelea wa kutoa makao kwa maskwota.