Aliyekuwa mwenyekiti wa chama cha TNA kaunti ya Nakuru Abdul Noor amemlaumu mbunge wa Nakuru Magharibi Samwel Arama kwa kuwa ‘fuko’ wa ODM kwenye Jubilee.
Noor amemchangamoto Arama kukoma kujihusisha na maswala ya chama kipya cha Jubilee Party of Kenya JPK, la sivyo ajiunge hadharani na chama hicho na kuondoka rasmi ODM.
Akiongea na wanahabari mjini Nakuru Jumanne, Noor alilalamika kwamba gavana wa kaunti ya Nakuru Kinuthia Mbugua na baadhi ya wabunge wanapanga kupendekeza viongozi wa chama hicho kwenye kaunti bila kushirikisha na kushauri wanachama kutoka vyama vingine vinavyounda Jubilee
“Lengo letu katika kuunda JPK, ni kuleta umoja wa jamii zote pamoja, na sio kugawanya wakenya kikabila kama inavyoonekana baadhi ya viongozi wa Nakuru wanafanya,” Noor alisema.
Noor alidai kwamba mkutano wa mashauriano uliofanyika katika hoteli moja ya Nakuru na kuongozwa na gavana Mbugua siku ya Jumamosi, ulinuiwa kuratibu jinsi ya kuzawadi wandani wao kisiasa nafasi za uongozi kwenye JAP, “ili wawasaidie kuomba kura katika uchaguzi wa 2017”.
Katika siku za hivi maajuzi Arama ameonekana kuunga mkono uongozi wa rais Uhuru Kenyatta akisema atashiriki katika kumsaidia kupigania kiti hicho ufikapo uchaguzi wa 2017.