Share news tips with us here at Hivisasa

Mamlaka ya Kitaifa ya Usafiri na Usalama nchini NTSA, imetambua maeneo matano ambayo yatawekwa vipima mwendo kwenye barabara kuu ya Nairobi-Nakuru.

Haya yamejiri huku mamlaka hiyo ikisema kuwa barabara hiyo ilikuwa ikiongoza kwa idadi za ajali zinazowalenga wapiti njia.

Maeneo hayo yaliyoteuliwa ni pamoja na Ihindu, Kinungi, Kayole, Mithuri na Karai, zote zikiwa mjini Naivasha, ambapo kumekuwa kukuripotiwa ajali nyingi.

Haya yameibuka baada ya maafisaa wakuu wa mamlaka hiyo pamoja na wale wa shirika simamizi la barabara za kitaifa KeNHA kuzuru maeneo hayo ambapo zaidi ya watu mia mbili wamepoteza maisha yao.

Akizungumza siku ya Jumatano, mwenyekiti wa NTSA Lee Kinyanjui alisema kuwa tayari wamemtambua mwanakandarasi atakayefanya kazi hiyo.

“Kazi ya kuweka vipima mwendo hivyo itafanyika katika kipindi cha siku tano kabla ya sikukuu ya krismasi ili kuweza kuzuia maafa wakati huo,” alisema Kinyanjui.

Mwakilishi wadi wa Naivasha Mashariki, Samuel Waithuki, amekaribisha hatua hiyo na kusema kuwa wakazi hususan wale wa Kinungi walikuwa wameadhiriwa na ajali hizo kwa miaka mingi.