Baadhi ya wasafiri katika Kaunti ya Mombasa wamepongeza shirika la uchukuzi na usalama barabarani (NTSA) kwa kufanya msako wa ghafla katika barabara ya Mbaraki jijini Mombasa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Mombasa siku ya Jumanne, Michael Murimi, ambaye ni afisa katika shirika hilo, alisema kuwa zoezi hilo linanuia kuondoa madereva ambao hawajahitimu kuendesha magari.
Murimi alisema kuwa madereva hao ndio husababisha ajali za mara kwa mara.
Akizungumza na mwandishi huyu, Said, ambaye ni dereva wa matatu, alisema kuwa anapongeza hatua hiyo kwani siku hizi madereva bandia wameongezeka barabarani.
Kwa upande mwengine, Kasyoki ambaye pia ni dereva, alisema kuwa zoezi hilo linawakandamiza na kuwaharibia biashara kwani wengi wao wameshikwa bila kosa lolote.
Hata hivyo, wasafiri wanaotembea kwa miguu wameitaka NTSA kuendeleza zoezi hilo katika kaunti nzima, ili kuregesha hali ya kawaida kwenye barabara.