Gavana wa Kaunti ya Nyamira John Nyagarama amelaumu serikali ya kaunti ya Kisii kwa kusimamisha kazi bodi ya maji eneo la Gusii bila kuhusisha serikali ya kaunti kwani serikali hiyo ina hisa zake kwa kampuni hiyo ya maji.
Kulingana na Nyagarama, aliyezungumza siku ya Jumapili mjini Nyamira, serikali ya kaunti ya Kisii ingefanya kikao na serikali ya Nyamira kwanza ili kutafuta suluhu halisi ikiwa wasimamizi wa bodi hiyo walikuwa na makosa kuliko kuchukua hatua peke yao bila kuhusisha serikali ya Nyamira.
“Serikali ya kaunti ya Nyamira ina hisa 11 katika kampuni ya 'Gusii Water and Sanitation' lakini tumesikia kuwa bodi inayosimamia kampuni hiyo imesimamishwa kazi na serikali ya Kisii bila kuhusisha serikali ya Nyamira,” alisema Nyagarama.
Kwa upande wa serikali ya kaunti ya Kisii, waziri wa maji katika kaunti hiyo Omoiro Omari aliyezungumza na waandishi wa habari Jumapili mjini Kisii, serikali ya kaunti iliamua kusimamisha kazi bodi hiyo kwa sababu bodi hiyo ilikataa kuandaa kikao na serikali hiyo kuzungumzia utata uliokuwa umekumba kampuni hiyo.
Waziri Omoiro alisema serikali ya Kisii ilikuwa na mamlaka ya kusimamisha bodi hiyo kazi kwani serikali ya kaunti ya Kisii ina hisa 89 kwa kampuni hiyo kuliko serikali ya Nyamira.