Gavana wa Kaunti ya Nyamira John Nyagarama ameombwa kuwachukulia hatua maafisa wa serikali ya kaunti ambao hawawajibikii kazi zao kama inavyostahili.
Wakizungumza siku ya Alhamisi mjini Nyamira, kiongozi wa wengi katika bunge la Kaunti ya Nyamira Laban Masira na kiongozi wa wachache katika bunge hilo Jackson Mogusu, walisema ikiwa maafisa wa serikali hawatafanya kazi jinsi inavyohitajika, basi serikali hiyo itakuwa imefeli katika maendeleo.
Viongozi hao walimwomba Gavana Nyagarama kuwachukulia hatua maafisa wanaoshindwa kufanya kazi.
Viongozi hao walisema wakuu wa idara na baadhi ya maafisa wa serikali hiyo ya kaunti hawafanyi kazi yao kikamilifu kwa njia ya haki na uwazi.
Walisema kuwa hali hiyo itaipa serikali ya Gavana Nyagarama jina mbaya, na kuchangia kushindwa kwake katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka wa 2017.
“Ikiwa wakuu wa idara na maafisa wa serikali watashindwa kufanya maendeleo, basi ni gavana ndiye atalaumiwa katika uchaguzi ujao na wala sio maafisa hao,” alisema Masira.
Aliongeza, “Ili kuzuia kulaumiwa, sharti gavana awachukulie hatua kali wale ambao hawawajibiki katika kazi zao, ili kuleta mabadiliko hapa Nyamira.”
Serikali ya Nyamira imekuwa ikilaumiwa kwa muda mrefu kwa kutoleta maendeleo kwa wakazi wa kaunti hiyo.
“Sisi tunahitaji kupongezwa kwa maendeleo wala sio kukosolewa kila mara. Hilo litafanyika ikiwa wakuu wa idara na maafisa wengine watashirikiana pamoja nasi kuleta maendeleo,” alisema Mogusu.