Mbunge wa zamani wa eneo bunge la Kitutu Masaba Mwancha Okioma amesuta vikali madai kuwa huenda akawa mwaniaji mwenza wa gavana John Nyagarama kwenye uchaguzi mkuu ujao.
Mbunge huyo wa zamani alisema kuwa iwapo atafanya hivyo, huenda akajiangamiza kisiasa huku akisisitiza kwamba yuko tayari kuwania ugavana na wala sio kuwa mgombea mwenza.
"Kamwe siwezi kuwa mgombea mwenza wa gavana Nyagarama, na iwapo nitafanya hivyo, hiyo itakuwa njia ya haraka yangu kuangamia kisiasa na mimi niko tayari kuwania ugavana na wala sio kuwa mgombea mwenza wa Nyagarama," alisema Okioma.
Hii ni baada ya mwanasiasa wa eneo hilo Evans Misati kusema kuwa Okioma ni msaliti kwa watu wa Bogetutu kwa kutaka kuwa mgombea mwenza wa gavana Nyagarama siku ya Jumapili alipowasihi wakazi wa Bogetutu kumpuuza.
"Kwa muda sasa nimekuwa nikiitwa msaliti kwa jamii ya watu wa Bogetutu, lakini hilo sio kweli kwa kuwa sijawahi fikiria kuwa mgombea mwenza wa mtu yeyote. Lengo langu ni kushirikiana na watu wa eneo hili kwa kuwa najua wapo tayari kunikabili mamlaka ya kuwa gavana wa Nyamira, na wale wanaoniharibia jina watashang'aa," aliongeza Okioma.
Okioma aliyekuwa akikutana na wazee wa eneo la Riakworo siku ya jumanne alisema kuwa kamwe hawezi jihuzisha na watu wafisadi.
"Jina langu ni safi na sitaki kujihuzisha na watu wafisadi kwa kuwa watu kufikiria kuwa naweza jiunga na gavana Nyagarama ni kama kuchanganya mafuta na maji ila sharti kuwa sharti nifanye kazi na serikali iliyoko kwa kuwa nikiwa upinzani haimaanishi kwamba ninapinga kila kitu," aliongezea.