Gavana wa kaunti ya Kisii James Ongwae amewaomba wakaazi wa kaunti hiyo kuwa na subira katika mradi wa ukarabati wa barabara.
Hii ni baada ya wakaazi wa kaunti hiyo kuendelea kuishinikiza serikali ya kaunti hiyo kuharakisha kuwakarabatia barabara haswa zile ambazo hazipitiki.
Kulingana na gavana Ongwae ni vigumu ukarabati wa barabara kuendelezwa ikiwa mvua inaendelea kunyesha ambayo inashukiwa kuwa ya gharika na kuomba wakaazi kusubiri hadi mvua itakapopungua.
Hata hivyo Ongwae aliahidi kukarabati barabara zile ziko katika bajeti ya mwaka wa 2015/2016 ili kurahisisha sekta ya uchukuzi kwa wafanyibiashara na wakulima.
Ongwae alisema tangu serikali yake iingie malmlakani imekuwa ikakarabati barabara kilomita 5 kwa kila wadi kila mwaka na kusema atajaribu kila awezalo kuhakikisha sekta ya uchukuzi haiwasumbui watu.
Ongwae alikuwa akiyaongea hayo siku ya Jumanne mjini Kisii huku akisema yuko tayari kuwatumikia wakaazi wa kaunti hiyo kimaendeleo.
Wakati huo huo, Ongwae alisema miradi ya maji itawekwa kila sehemu ya kaunti kuwarahisishia kazi akina mama ambao hutembea mbali kutafuta maji.
“Serikali yangu itaweka miradi ya maji kila sehemu hapa Kisii, tayari tumeweka miradi ya maji 21 na visima 24 vinaendela kuchimbwa,” alisema Ongwae.