Share news tips with us here at Hivisasa

Mkewe gavana wa kaunti ya Kisii Bi Elizabeth Ongwae amefadhili shule tano za msingi katika eneo bunge la Kitutu Chache kaskazini vitabu vya kusoma ili kuinua viwango vya elimu.

Baadhi ya shule ambazo zilikabidhiwa vitabu hivyo ni shule ya msingi ya Samugara, Kioge, Kenyoro, Gesangero, na Omogumo ambazo ziko katika eneo bunge hilo la Kitutu Chache.

Msaada huo wa vitabu ulijiri baada ya shule hizo kukiri kuwa hazina vitabu vya kutosha, na ndiposa Ongwae, kwa ushrikiano na chama cha Scoop International aliamua kujitolea kutoa usaidizi huo kama njia moja ya kuinua viwango vya elimu katika Kaunti ya Kisii

Aidha, Ongwae aliwaomba wazazi wote, walimu, wanafunzi na washikadau wengine katika eneo bunge hilo kuungana na kushirikiana pamoja kuhakikisha viwango vya masomo vimeinuka.

“Nimekuja hapa kukabidhi shule hizi vitabu kama njia moja ya kuinua viwango vya elimu juu,” alisema Ongwae.

“Nahitaji watoto wetu wajue kusoma na kuongea kizungu, naomba tuweze kuona furaha kwa wanafunzi na kwa wazazi wao wakifurahia matokeo mazuri ya mitihani ili kaunti yetu ya Kisii iwakilishwe na shule za eneo bunge hili kwa kufanya vizuri katika mtihani wa kitaifa,” aliongezea.

Idadi nyingi ya wazazi wa shule hizo walimpongeza Ongwae kwa kazi anayoifanya, na kusema kuwa wako tayari kufanya kazi naye ili kuinua viwango vya elimu zaidi.