Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Maafisa wawili wa polisi wanapokea matibabu katika hospitali kuu ya wilaya ya Molo, baada ya kuhusika kwenye ajali iliyotokea Jumatatu eneo la Nyanja kwenye barabara kuu ya Nakuru-Eldoret.

Wawili hao, mmoja kutoka kitengo cha idara ya misitu (KFS) na mwingine wa idara ya ujasusi (CID) wamenusurika kifo baada ya gari walilokuwa wakisafiria kupoteza mwelekeo na kubingiria mara kadhaa.

Walioshuhudia ajali hiyo walisema gari la polisi aina ya Toyota Land Cruiser lilikuwa likiendeshwa kwa mwendo kasi kabla ya dereva kupoteza udhibiti wake.

''Gari lilikuwa likiendeshwa kwa kasi na tukiwa upande ule wa pili wa barabara tuliona limebingiria na kisha kuingia kwa mtaro” akasema Ibrahim Kendi.

Kumekuwa na ongezeko la ajali kwenye barabara kuu ya Nakuru kwenda Eldoret huku madereva wakitakiwa kuwa wangalifu haswa msimu huu wa sherehe.

Ajali hiyo imedhibitishwa na kamanda wa trafiki wilayani Molo Nderitu Maina ambaye amesema maafisa waliohusika kwenye ajali ni wa kutoka kituo cha polisi cha Londiani.

"Tunawaomba madereva kutii sheria na alama za barabarani ili kuepuka maafa yanayoweza kuzuiliwa." akasema Maina.

Gari hilo limekokotwa hadi kituo cha polisi cha Mau Summit.

Kwingineko watu wawili walipoteza maisha yao kufuatia mkasa wa ajali kwenye matukio mawili tofauti barabarani mjini Naivasha na viungani mwake Jumatatu.

Katika kisa cha kwanza mwanamme mmoja amefariki baada ya kugongwa na gari lililokuwa likiendeshwa kwa kasi katika eneo la Kinungi kwenye babara kuu ya Naivasha kuelekea Nairobi.

Dereva wa gari lililosababisha ajali hiyo aliepuka kifo mikononi mwa wakaazi waliojawa na gadhabu wakitaka kumpatiliza kichapo cha mbwa, lakini akaokolewa na polisi.

Na katika kisa cha pili mwanamme mwingine aliaga dunia baada ya gari lake kugongana ana kwa ana na trela kwenye barabara kuu ya Mai Mahiu kuelekea Naivasha.

Afisaa mmoja wa polisi wa ngazi ya juu na ambaye hakutaka kutajwa jina lake amedhibitisha matukio hayo mawili akisema, "Uchunguzi umeanzishwa na miili yote miwili imepelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali kuu ya wilaya ya Naivasha.”

Eneo la Kinungi linajulikana kutokana na wingi wa ajali, huku wakaazi wakiitaka serikali kushibiti idadi ya maafa yanayotokea eneo hilo.