Idara ya polisi katika Kaunti ya Mombasa imetangaza vita dhidi ya kundi lijulikanalo kama Wakali Kwanza.
Kundi hilo linadaiwa kuhangaisha wakazi katika eneo la Kisauni kwa muda sasa kwa kuzua vurugu sawia na kutekeleza visa kadhaa vya wizi wa mabavu.
Kamanda wa polisi katika eneo la Pwani, Francis Wanjohi, alisema kuwa huenda usumbufu wa kikundi hicho ukakomeshwa kufikia mwezi Februari mwakani baada ya idara ya usalama katika Kaunti ya Mombasa kutangaza vita dhidi ya kikundi hicho.
“Hatutaruhusu kikundi hiki kuendelea kuhangaisha wakazi. Idara ya usalama itahakikisha imekabiliana nao vilivyo kufikia mwakani,” alisema Wanjohi.
Akizungumza katika kikao na wanahabari katika eneo la Pirates katika ufuo wa bahari ya umma wa Jomo Kenyatta siku ya Jumatatu, Wanjohi alisema kuwa msako umeanzishwa kukabiliana na kikundi hicho ambacho wakazi wengi wa maeneo ya Kisauni wamekitaja kama mwiba kwenye eneo hilo.
Wanjohi aidha aliwahakikishia wakazi kuwa usalama utaimarishwa msimu huu wa likizo.
Hata hivyo machifu wamearifiwa kuimarisha utendakazi wao na kutoa taarifa muhimu kwa maafisa wa usalama kuhusiana na swala hilo, kwa kuwa wako karibu zaidi na makazi ya wahalifu hao.
Vile vile, wazazi wametakiwa kuwa mstari wa mbele katika kutambua mienendo ya wanao na kuwapa muongozo bora ili kuwaepusha kujiunga na vikundi vya uhalifu.