Share news tips with us here at Hivisasa

Mahakama kuu ya Mombasa imewahukumu kifungo cha miaka saba maafisa wawili wa polisi waliopatikana na makosa ya mauaji bila kukusudia ya mtoto wa miaka 14, Kwekwe Mwandaza.

Akitoa hukumu hiyo siku ya Jumatatu, jaji katika mahakama kuu ya Mombasa Martin Muya alisema kuwa sharti polisi wanaotumia silaha vibaya wakabiliwe kisheria na kuitaka hukumu hiyo kama funzo kwa wengine.

Aidha, alitaja kuwa kuna visa vingi vya polisi kushiriki katika utumizi mbaya wa silaha kwa wananchi wasiokuwa na hatia nchini, na kuitaka idara ya polisi kuwachukulia hatua maafisa kama hawa.

Wawili hao wako na siku 14 ya kukata rufaa kupinga hukumu hiyo.

Aidha, Muya ametupilia mbali ombi la kuwataka washukiwa hao kulipa fidia kwa kusema kuwa hawana uwezo na kuongeza kuwa serikali bado haijatenga pesa za kufidia.

Vile vle, ameitaka serikali kuunda kitengo cha kushughulikia ulipaji fidia kwa wahanga wa dhulma nchini.

Wiki iliyopita, jaji Martin Muya aliwapata na kosa la mauwaji bila kukusudia maafisa Veronica Gitai na Issa Mzee.

Afisa wa upelelezi Veronicah Gitahi pamoja na Issa Mzee wanadaiwa kumpiga risasi mtoto wa miaka 14 Kwekwe Mwandaza Agosti 22,2014 katika kijiji cha Maweu huko Kinango kaunti ya Kwale.