Share news tips with us here at Hivisasa

Polisi katika eneo la Makutano kaunti ndogo ya Mwala hapo siku ya Ijumaa walilazimika kufyatua vitoa machozi ili kutawanya umati wa wakaazi uliokuwa na ghadabu na kutaka kumteketeza mwanamke mmoja kwa madai ya kuwa mhusika mkuu kwa mauaji yanayotekelezwa katika eneo hilo. 

Wakaazi hawa walidai kuwa mwanamke huyo ambaye huendeleza biashara ya kilabu hutumia nguvu za gizani ambapo walidai alihusika kwa njia moja au nyingine katika mauaji ya watu yanayotekelezwa katika eneo hilo. 

Kwa mujibu was mkuu wa polisi wa kaunti ndogo ya Mwala Henry Rukaria, alisema kuwa maafisa was polisi walipata habari mwendo wa saa mbili usiku kuwa kulikuwa na vurugu katika soko hilo pale walifika na kuwapata wakaazi wamewasha moto nje ya kilabu cha mwanamke huyo tayari kumchomea ndani. 

Rukaria alisema kuwa mwanamke huyo alikuwa amepiga ripoti siku chache zilizopita akidai kutishiwa maisha yake pale alikuwa akiambiwa ahame eneo hilo la sivyo atakiona cha mtema kuni. 

Aidha afisa huyo alisema kuwa polisi wameanzisha uchunguzi ili kubaini iwapo mwanamke huyo alihusika katika vifo hivyo kama wakaazi walivyodai. 

Haya yanajiri wiki tatu baada ya mwanamume wa umri wa makamo alipatikana ameaga katika nyumba moja iliyotengwa katika eneo hilo pale wazee wengine wawili waliuwawa na watu wasiojulikana na miili yao kutupwa katika eneo la Nunga visa ambavyo viliwatia wenyeji tumbo joto.