Mshukiwa mmoja ambaye anadaiwa kuwa kiongozi wa mtandao wa kuuzia wanafunzi wa chuo kikuu cha Moi kitivo cha sheria bangi ametiwa mbaroni.
Mshukiwa huyo alitiwa mbaroni karibu na bewa la Annex la chuo kikuu cha Moi ambapo huendelezea biashara yake.
Juhudi za mshukiwa huyo kutoroka kwa kutumia pikipiki ziliambulia patupu kwani aliandamwa na maafisa wa polisi wa utawala kwa ushirikiano na maafisa wa bodi ya kukabiliana na pombe na dawa za kulevya katika kaunti ya Uasin-Gishu kabla ya kumvumania na kumtia mbaroni.
Mkurugenzi wa bodi hiyo Bw Armstrong Rono alidhibitisha kuwa mshukiwa huyo alinaswa na misokoto zaidi ya 100 ya bangi ya kima cha shilingi 40,000.
“Tumekuwa tukimsaka huyu mshukiwa kwa muda mrefu ,amekuwa akiuuzia wanafunzi bangi,bangi hii imeaathiri wanafunzi wengi sana,kuwepo kwa dawa za kulevya kwa wingi katika eneo hili kumechangia kudorora kwa usalama katika chuo cha biashara cha Annex mbali na ukosefu wa nidhamu miongoni mwa wanafunzi husika.” Alisema Rono
Akihutubia wana habari katika kituo cha polisi Kiambaa Bw Rono alisema ongezeko la biashara haramu ya dawa za kulevya katika maeneo ya karibu na chuo hicho limechangia katika ongezeko la visa vya kudorora kwa usalama katika maeneo ya akribu na chuo hicho mbali na kuathiri ufanisi wa wanafunzi masomoni.
Bw Rono alisema maafisa husika wamekuwa wakimsaka mshukiwa kwa muda mrefu ambapo amekuwa akiwakwepa kwa kutumia pikipiki.
Bw Rono aliongeza kwamba bodi yake imejitolea kukabiliana na walanguzi wa dawa za kulevya katika kaunti ya Uasin-Gishu.
Tayari mshukiwa amefikishwa katika mahakama ya kaunti mjini Eldoret kujibu mashtaka ya kuuzia wanafunzi bangi.