Polisi jijini Kisumu walipata bunduki moja aina ya AK 4 siku ya Alhamisi, katika eneo la kutupa taka la Kachok, karibu na uga wa Michezo wa Moi jijini Kisumu.
Akidhibitisha kisa hicho, Mkuu wa wilaya ya Kisumu Mashariki Moses Ole Tutui, alisema kuwa waliarifiwa kuhusu bunduki hiyo na wakazi wa eneo hilo.
“Wakazi wa eneo hili ndio waliotusaidia. Walipoiona bunduki hiyo ikiwa imefichwa ndani ya taka, walinipigia simu na tukaja kuichukua,” alisema Ole Tutui.
Inashukiwa kuwa bunduki hiyo imekuwa ikutumika kutekeleza uhalifu jijini Kisumu.
Mkuu huyo wa polisi alisema kuwa bunduki hiyo ilipatikana ikiwa na risasi kumi na mbili, ishara kwamba risasi kumi na nane zilikuwa tayari zimetumika.
Ole Tutui alitoa wito kwa wananchi, kushirikiana na idara ya usalama katika kutokomeza uhalifu jijini Kisumu.
Alisema kuwa uchunguzi wa kina umeanzishwa, ili waliokuwa na bunduki hiyo wakamatwe na kufunguliwa mashtaka.