Mwakilishi wa wadi ya Bahati katika bunge la kaunti ya Nakuru Peter Nderitu, amepongeza idara ya polisi kwa kuharakisha kumtia mbaroni Rubani aliyemdhalilisha afisa mmoja wa polisi wa kike Mercy Wandera katika eneo la Ndunyu Njeru, Nyandarua.
Nderitu amesema ni lazima wananchi na wageni watii sheria za taifa, pamoja na mamlaka polisi waliopewa iwe ni wa kike ama kiume.
Ni vyema kwa sababu wananchi hawakuchukua sheria mikononi mwao kumwadhibu rubani huyo, na pia wale walionasa hiyo video walifanya vizuri. Lakini kongole zaidi ni kwa inspekta Jenerali mkuu wa polisi Joseph Boinnet aliyetoa taarifa mara moja kukemea kitendo hicho, na kuamuru jamaa huyo akamatwe,” alisema Nderitu akizungumza na mwandishi huyu.
Rubani huyo Lewelyn Alistar Patrick Jumatano alifikishwa mbele ya mahakama moja ya Kinangop na kukabiliwa na mashtaka mawili.
Mbele ya hakimu mkuu mkazi wa Engineer Martin Mutegi, Patrick alikabiliwa na mashtaka ya kumpacha askari huyo pamoja na kuzua rabsha. Aliwekwa rumande hadi Jumatatu Feb 29, 2016 ambapo kesi hiyo itarejelewa.
Upande wa mashtaka ukiongozwa na George Mung’are ulipinga kuachiliwa kwa mshukiwa kwa dhamana, akisema kuwa huenda akatoroka humu nchini.
Mshukiwa anawakilishwa na wakili Stanley Kang’ahi.