Idara ya usalama katika eneo la Pwani imeshinikizwa kuhakikisha kuwa inatuma maafisa zaidi wa usalama katika eneo bunge la Malindi, ili kuhakikisha kuwa mchakato wa kisiasa na kampeni zinaozendelea kwa sasa haziwagawanyi Wakenya.
Mchanganuzi wa maswala ya kisiasa katika eneo la Pwani Wakili Johnson Muchiri amesema kuwa kila mrengo wa kisiasa unatarajiwa kuonyesha ubabe wake wa kisiasa lakini itakuwa vyema iwapo maafisa wa usalama watashika doria kuzuia kutokea kwa vurugu.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Muchiri alisema kuwa kuna haja ya usalama kuimarishwa kwa manufaa ya wakazi wa eneo hilo na ukanda wa Pwani kwa jumla ili kuhakikisha kuwa kampeni hizo zinafanyika kwa amani na uchaguzi huru usioegemea upande wowote.
"Idara ya usalama lazima itume maafisa wake eneo bunge la Malindi kushirika doria kikamilifu na kuzuia kushuhudiwa malumbano na mgawanyiko kwa wakaazi kutokana na mchakato wa kisiasa unaoendelea eneo la Malindi,” alisema Muchiri.
Wakati uo huo wamewataka viongozi wa kisiasa wanaoendeleza kampeni zao za kuwapigia debe wafuasi wao kuhakikisha kuwa wanaendesha siasa zao kwa njia ya amani na kujitenga na siasa za uchuki na uchochezi ili kuzuia kuwagonganisha Wakenya.
Uchaguzi huo mdogo wa Malindi wa kuziba nafasi iliyowachwa wazi na Dan Kazungu aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Madini utafanyika tarehe Machi 7 kama ulivyopangwa na Tume ya IEBC.