Share news tips with us here at Hivisasa

Kamanda mkuu wa trafiki eneo la Pwani Martin Kariuki amesema kwamba polisi wa trafiki zaidi wametumwa katika eneo la Taru kudhibiti msongamano wa magari unaoshuhudiwa katika eneo hilo.

Kariuki alisema kuwa maafisa hao waliotumwa katika eneo hilo lililoko kwenye barabara kuu ya Mombasa-Nairobi watazindua mbinu mpya za kuongoza magari ili kukabiliana na msongamano huo.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Ijumaa, Kariuki alisema kwamba magari yatalazimika kutumia barabara ya reli inayojengwa katika eneo hilo ili kuudhibiti msongamano huo.

Afisa huyo alisema kwamba hali hiyo imechangiwa na shughuli za ujenzi wa barabara  zinazoendelea katika eneo hilo la Taru, sambamba na shughuli za ujenzi wa reli, ambazo zimeathiri shughuli za uchukuzi.

“Tumetuma maafisa zaidi wa trafiki kuongoza magari na kupunguza msongamono huo ambao umetokana na ukarabati wa barabara ya Mombasa-Nairobi katika eneo la Taru, haswa baada ya mvua kunyesha,” alisema Kariuki.

Siku tatu zilizopita, mamia ya abiria walikwama katika barabara hiyo kwa muda wa siku mbili mtawalia baada ya mvua kubwa kunyesha na kukatiza shughuli ya ujenzi wa barabara na kusababisha msongamano mkubwa katika barabara hiyo.