Share news tips with us here at Hivisasa

Kiongozi wa upinzani Raila Odinga amedai kuwa mrengo wa Jubilee unatumia miradi ya Shirika la huduma kwa vijana NYS kusaka wafuasi ili wasalie uongozini ifikiapo mwaka wa 2017.

Raila, ambaye pia ni kinara wa mrengo wa Cord amewataka Wakenya kutoiona serikali ya Jubilee inayoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta kama serikali ya kielelezo chema, huku akidai kuwa haijatimiza ahadi walizozitoa kuhusu kupambana na ufisadi nchini.

“Jubilee imevunja ahadi zake zote kuhusu kupigana na ufisadi. Tusishawishike kuunga mkono mienendo yao ambayo imedhibitisha wazi kuwa ni ya kupotosha nchi ya Kenya,” alisema Raila.

Akizungumza katika Kaunti ya Kisii siku ya Alhamisi, Raila aliziagiza serikali za kaunti kutoiga mienendo ya serikali kuu huku akiongeza kuwa mrengo wa Cord hautakubali matumizi mabaya ya fedha za umma, ufisadi na kutowajibika kwa serikali yoyote ya kaunti.

“Serikali za kaunti zafaa kutilia maanani miradi ya maendeleo ya kuwasaidia Wakenya. Iwapo Cord wataingia serikalini mwaka wa 2017, tutahakikisha kila mtu amewajibikia mali ya umma iliyoibwa,” alisema Raila.

Raila alisema kuwa mrengo wa Cord utadhibitisha kuwa kuna uwezekano wa kuwepo kwa serikali huru na ya ukweli, ambayo Wakenya wameisubiri kwa muda mrefu.