Share news tips with us here at Hivisasa

Gavana wa kaunti ya Mombasa Ali Hassan Joho anazidi kumiminiwa sifa na viongozi wa upinzani kwa kile wamekitaja kama tendo la kishujaa baada ya Joho kuonyesha msimamo dhabiti mbele ya viongozi wa Jubilee. 

Katika mahojiano na gazeti moja la humu nchini siku ya Jumapili, kiongozi wa upinzani Raila Odinga alimtaja Joho kama kiongozi asiye babaishwa na mawimbi ya Jubilee huku akiutaja msimamo wake kuwa ishara tosha kuwa mkoa wa Pwani ungali ngome ya upinzani. 

''Aliwadhihirishia kuwa Pwani inaunga mkono Cord na kuwa wakaazi wa Mombasa wanakipenda chama cha ODM ndiyo maana walimchagua Joho kuwa gavana wao,'' alisema Raila. 

Raila alidai kuwa Jubilee inatumia pesa kuwahonga baadhi wa viongozi wa upinzani kutoka mkoa wa Pwani ili wajiunge nao katika uchaguzi wa 2017.

Tayari viongozi kadhaa kutoka mkoa wa Pwani wakiongozwa na mbunge wa Likoni Masoud Mwahima wametangaza kuhamia Jubilee na kusema kuwa watavitetea viti vyao katika uchaguzi ujao kwa tiketi ya chama cha JAP. 

Wengine waliompongeza Joho ni wabunge Junet Mohammed (Suna Mashariki) na Millie Odhiambo (Mbita). 

''Joho, wewe ni shujaa wangu wa siku, umesimama wima mbele yao na kuwaambia ukweli bila uwoga. Heshima nakupa,'' alisema Millie. 

Siku ya Jumamosi katika hafla ya kuwapa hati miliki maskwota wanaoishi katika shamba la Waitiki, Likoni, gavana Joho alimwambia Seneta wa Nairobi Mike Sonko kuwa hawezi iipigia kampeni mrengo wa Jubilee. 

''Sonko, wacha nikwambie, mimi ni mwanachama wa ODM kwa hivyo usitarajie nikupigie kampeni. Nitakipigia debe chama changu na wewe pia fanya hivyo, hiyo ndiyo demokrasia,'' alisema Joho.