Share news tips with us here at Hivisasa

Kiongozi wa chama cha upinzani cha Cord Raila Odinga ameiomba serekali kuwapa wanahabari uhuru wa kutangaza habari na kusita kuwapa vitisho kila mara.

Mwenyekiti huyo wa chama cha ODM alighadhabishwa na hatua ya kushikwa kwa mwanahabari wa Kituo cha Nation John Ngirachu, kufuatia amri ya Waziri wa Usalama wa Ndani nchini Joseph Nkaiseri baada ya Ngirachu kuchapisha habari iliyofichua taarifa ya ufisadi katika wizara hiyo.

Kupitia mtandao wake wa Facebook siku ya Jumanne, Odinga aliwapa pole familia na marafiki wa Ngirachu na wanahabari kwa jumla huku akiitaka serikali iheshimu kazi ya wanahabari.

"Nachukua fursa hii kuiomba serikali kuheshimu wanahabari kwa vile wana kila sababu ya kuficha watu waliowapa ujumbe waliochapisha. Hii si mara ya kwanza tumeshuhudia visa kama hivi na hili linaturudisha nyuma kama taifa,” alielezea Odinga.

Ngirachu alichapisha taarifa ambazo zilihusisha Wizara ya Usalama na Masuala ya Ndani na ufisadi wa Sh3.5bn, hatua iliyopelekea Nkaiseri kumwagiza ataje waliomfichulia habari hizo la sivyo atiwe mbaroni.

Odinga hata hivyo alimhakikishia Ngirachu kuwa chama chake kitamuunga mkono na kuhakikisha anaendelea na kazi yake kama kawaida.

“Kama chama pinzani tutamuunga mkono Ngirachu hadi pale atakapoachiliwa huru na kuruhusiwa kuendelea na kazi yake. Lazima Kenya isonge mbele kimaendeleo, uhuru na usawa,” alisema Odinga.

Ngicharu aliaachiliwa baada ya kuandikisha taarifa na maafisa wa uchunguzi wa jinai kuhusu taarifa hizo.