Mbunge wa eneo bunge la Nakuru Magharibi Samuel Arama amesema kiongozi wa Cord Raila Odinga ni rafiki yake mkubwa wala hana chuki na ugomvi naye.
Akizungumza siku ya Ijumaa alasiri katika uwanja wa marafuu viungani mwa mji wa Nakuru, wakati alipopeana hundi za uwezo kwa vikundi mbalimbali pamoja na za basari ya jumla ya shilingi milioni 15, mbunge huyo amesema kinacholeta tofauti kati yake na Raila Odinga ni maoni.
Arama ameongeza kuwa kila mtu ana uhuru wa kujieleza na kutoa maoni yake, jambo ambalo amesema linakubalika kwa mujibu wa katiba.
Ijapo kuwa Arama ambaye alichaguliwa kwa tiketi ya chama cha ODM na kuonekana siku za hivi maajuzi kutofautiana na kinara huyo, amesema kuwa yeye huomba ushauri sawa na kusemezana na kiongozi huyo wa upinzani kwa minaajili ya maendeleo ya eneo hilo.
Isitoshe amesisitiza ya kuwa kufanya kazi na serikali iliyo mamlakani kwa sasa haimaanishi amehama chama cha ODM.
Hata hivyo amewataka wale ambao wananuia kuwania kiti cha ubunge cha Nakuru magaribi, kutafuta mbinu mpya ya kuwarai wapiga kura wa eneo hilo badala ya kumchafulia jina ya kwamba amehama chama cha ODM.
Ameshikilia ya kwamba ataendelea kuwahudumia watu wa eneo hilo akiwa ndani ya chama cha ODM, hadi mwaka ujao 2017, wakati wa uchaguzi mkuu ambapo atatafuta ushauri kutoka kwao, na ni tiketi ya chama kipi atakayo tumia kutetea kiti cha eneo hilo.