Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Rais Uhuru Kenyatta amekosolewa na viongozi mbalimbali wa mashirika ya kijamii kwa kutoangazia vyema usawa wa jinsia katika shughuli ya uteuzi wa baraza la mawaziri nchini.

Mashirika hayo, yakiongozwa na shirika la kutetea haki za kibinadamu nchini la Haki Afrika, yamesema kwamba baraza la mawaziri lililoteuliwa hivi majuzi halikuzingatia usawa wa jinsia katika uteuzi huo jinsi katiba inavyoangazia nchini.

Afisa mratibu wa mipango katika Shirika hilo Francis Auma Gamba alisema kwamba kati ya mawaziri ishirini ambao rais aliwateuwa, wanne pekee ndio mawaziri wanawake licha ya katiba kuangazia vyema usawa wa jinsi katika uongozi nchini.

Kwenye mahojiano ya kipekee na wanahabari wetu afisini mwake siku ya Jumamosi, Gamba alisema kwamba serikali imeonyesha wazi kuwa katiba haina umuhimu, na wakenya waliipigia kura ili kutumika katika maswala ya uongozi nchini, hivyo basi hatua ya rais inafaa kukosolewa.

“Tumeona wazi kuwa rais mwenyewe hakuzingatia katiba alipokuwa akifanya uteuzi wa baraza la mawaziri baada ya kuona wazi kuwa maziri alionao ni wafisadi, tunaipongeza hatua hiyo lakini tunataka kuona katiba ikiheshimiwa hapa nchini na haswa wa kwanza kuheshimu katiba ni rais wetu ndio atafanya kila mwananchi kuheshimu katiba,” alisema Gamba.

Rais Kenyatta alilifanyia mabadiliko baraza lake la mawaziri nchini baada ya kushinikizwa na viongozi wa upinzani, mashirika ya kijamii na wananchi kutokana na baadhi ya mawaziri kukumbwa na kashfa ya ufisadi katika wizara zao.