Rais Uhuru Kenyatta amemtaka mkurugenzi mkuu mpya wa Vijiana wa Huduma kwa Taifa NYS kuanza kazi na kuhakikisha malengo ya shirika hilo la serikali yanafanikishwa na kulainisha shirika hilo ambalo limekuwa kwenye zimwi la ufisadi katika siku za hivi karibuni.
Akitoa hotuba yake kwa nchi katika ikulu ya Mombasa siku ya Jumanne, Rais alisema kuwa serikali yake inafanya juhudi ili kuona kuwa shirika hilo linakuwa na hadhi yake na kusema kuwa wataendelea kupigana na mienendo mibaya miongoni mwa maafisa wasiofuata utaratibu unaokubalika kisheria.
Kwenye hotuba yake Rais alimtaka afisaa huyo Richard Ethani Ndubai kutumia tajiriba na ujuzi kwenye sekta ya umma kuleta nidhamu pamoja na kujenga jina la shirika hilo na kuwafaidi vijana wanaojiunga na shirika hilo kila mwaka.
Kwa upande wake mkurugenzi huyo mpya huku akisoma akikula kiapo cha kuchukua nafasi hiyo, alisema kuwa atafuata sheria na kuleta ujuzi wake kwenye shirika hilo la NYS.
Itakumbukwa kuwa aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa shirika hilo Nelson Githinji alijiuzulu baada ya shirika hilo kukumbwa na madai ya ufisadi ambayo pia yalimsababisha waziri wa ugatuzi ambako shirika hilo la NYS liliwajibishwa kwayo Ann Waiguru kujiuzulu mwezi uliopita.
Wengi wa Wakenya watangoja kuona kama afisaa huyo ataleta ulainishaji wa shirika hilo la Huduma kwa Taifa.