Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho anadai kuwa Rais Uhuru Kenyatta amekuwa akimkwepa mara kwa mara tangu azuru Mombasa mapema wiki hii kwa ziara rasmi. 

Share news tips with us here at Hivisasa

Joho anadai hadi sasa hajakutana na Rais kwani hajaalikwa wala kufahamishwa kuhusu shughuli zake licha ya kiongozi wa nchi kuwa Mombasa kwa siku nne sasa. 

''Sijui lolote kuhusu ziara ya Rais, sijui ako Mombasa sehemu gani lakini nasikia wamekuwa wakizunguka mjini,'' alisema Joho. 

Joho anadai amekuwa akilengwa mara kwa mara kutokana na msimamo wake dhabiti kuhusu serikali na pia kuwa yeye ni miongoni mwa viongozi wakuu wa upande wa upinzani. 

''Hawana nia njema na Mombasa, sijashangaa na haya sababu sikutarajia mapya kutoka kwao,'' alisema Joho. 

Tangu aanze ziara yake ya wiki moja mjini Mombasa, Rais hajaonekana akitangamana na viongozi wakisiasa wa kaunti ya Mombasa isipokuwa Jumanne usiku alipoandamana na mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir alipozuru Fort Jesus, mtaa wa Old Town, Majengo Saba Saba na Buxtan. 

Siku ya Jumatatu, Rais alifanya ziara ya ghafla katika kivuko cha Feri ya Likoni kabla kukutana na viongozi wa kaunti ya Lamu baadaye katika Ikulu ya Mombasa. 

Siku ya Jumatano Rais aliandaa kikao na zaidi ya vijana 600 katika Ikulu ambapo pia viongozi kutoka kaunti za Tana River, Lamu, Kilifi, Kwale na Taita Taveta walihudhuria. 

Wadadisi wa kisiasa sasa wanadai kukosekana kwa Gavana Joho na Seneta wa kaunti ya Mombasa katika ziara ya Rais mjini humo, kunaashiria uhusiano baridi ulioko baina ya viongozi hao na uongozi hususan baada ya Joho kunukuliwa Desemba 13,2015 katika mkutano moja mjini Mombasa akisema Uhuru ajipange kuwa katika upinzani baada ya uchaguzi wa 2017.

Hata hivyo, idara ya mawasiliano ya Rais haijatoa taarifa zozote kuhusu suala hilo.